Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (a.s) -ABNA- Hujjatul-Islam wal-Muslimin Basim Al-Shar’i, Imam wa Ijumaa wa jimbo la Michigan, Marekani, katika hotuba ya Ijumaa wiki hii alisisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imepata “ushindi mkubwa na wa kutukuka” katika vita vya siku kumi na mbili vilivyoanzishwa na utawala wa Kizayuni dhidi yake, na iliweza kulinda maslahi yake ya kitaifa bila kutegemea nguvu za mataifa ya kigeni.
Al-Shar’i akizungumzia zaidi ya miongo minne ya shinikizo na vikwazo dhidi ya Iran alisema:
“Iran, licha ya miaka arobaini ya kuzingirwa na bila msaada wa China, Russia au nchi nyingine yoyote, imeweza—kwa kutegemea uzalishaji wa ndani, uamuzi wenye hekima na uimara wa wananchi wake—kudhibiti tishio la nje kwa ujasiri na busara.”
Imam huyo wa Michigan alibainisha kuwa taasisi za utafiti duniani kwa sasa zinachunguza namna ushindi huo ulivyopatikana na zinatilia mkazo nafasi muhimu ya uongozi katika mafanikio hayo.
Aliongeza:
“Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, ni shahsi wa kimataifa ambaye kauli na misimamo yake huzingatiwa na taasisi nyingi duniani. Hekima yake, wepesi wa kufanya maamuzi na uwezo wake wa kusimamia misukosuko ni sifa zilizomfanya aendelee kuheshimiwa duniani akiwa na umri wa karibu miaka tisini.”
Al-Shar’ alionyesha masikitiko kuhusu baadhi ya ukosoaji uliojitokeza ndani ya Iran baada ya vita kumalizika na akautaja mtazamo huo kuwa “wenye kuleta changamoto na kudhuru utulivu wa ndani.”
Akasema:
“Kwa bahati mbaya, baadhi ya viongozi wa zamani wa serikali ambao walikuwa madarakani kwa miaka mingi, baada ya kumaliza muda wao wameanza kutupa lawama na kutoa maneno ya mafumbo dhidi ya uongozi. Hili linaathiri afya ya mazingira ya ndani ya Iran.”
Imam wa Michigan alisisitiza kuwa hatari kuu kwa Jamhuri ya Kiislamu inatokana na mambo ya ndani, si ya nje, na akaongeza:
“Nguvu ya wananchi wa Iran imo katika umoja wao na kushikamana kwao na uongozi wenye busara wa Ayatullah Khamenei. Umoja huu ndiyo heshima na mtaji wa kweli wa Jamhuri ya Kiislamu.”
Akigusia tofauti ya kimtazamo kati ya fikra ya Kiislamu na ile ya Magharibi, alisema:
“Magharibi inataka maadili yatumike kuutumikia ulimwengu wa siasa, ilhali Jamhuri ya Kiislamu — kwa mujibu wa mafundisho ya Uislamu — inaifanya siasa itumike kuimarisha maadili. Tofauti hii ni ya kimsingi na ya kimaumbile.”
Mwisho wa hotuba, alitoa wito kwa makundi yote ya kisiasa kuepuka mvutano na badala yake kuzingatia mshikamano, akisisitiza:
“Leo dunia inasoma kauli za Kiongozi wa Mapinduzi na kuziwekea tafiti maalumu. Naomba Mwenyezi Mungu amlinde Kiongozi Muadhamu, Marjaa na wanazuoni wa Umma wa Kiislamu.”
Your Comment